23 Mei 2021 - 13:09
Mripuko wa volkano mashariki DRC, maelefu wakimbia Goma

Mripuko hatari wa volkano ambao umeandamana na lava umeripotiwa katika Mlima Nyiragongo Jumamosi usiku mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa taarifa, lava kutoka mlipuko huo wa volkano inaripotiwa kuelekea katika uwanja wa ndege wa Goma, ambao ni mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC.

Serikali imetoa wito kwa watu kuhama haraka katika mji huo wenye watu milioni mbili na tayari maelefu ya watu usiku wa kuamkia leo wameonekana wakikimbia kwa miguu kuelekea mpaka baina ya nchi hiyo na Rwanda.

Volkano ya Mlima Nyiragongo ililipuka mara ya mwisho mwaka 2002 na kuua watu 250 huku wengine zaidi ya 120,000 wakiachwa bila makao. Mlima huo una moja ya volkano hai  na hatari zaidi duniani.

Wizara ya Masuala ya Dharura nchini Rwanda imesema hadi sasa Wakongomani zaidi ya 3,500 wameshavuka mpaka na kuingia nchini humo ambapo wanapewa hifadhi katika shule na maeneo ya ibada.

Taarifa zinasena awali lava ya volkano hiyo ilionekena ikielekea Rwanda lakini sasa inaelekea kati kati ya mji wa Goma.

Hata hivyo, Celestin Kasereka mkuu wa utafiti katika Kituo cha Kuchunguza Volkano Goma amesema hadhani lava hiyo ina kasi ya kutosha ya kufika Goma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  Jean-Michel Sama Lukonde  ameitisha kikao cha dharura mjini Kinshasa na serikali inatayarisha mpango wa kuwahamisha kwa haraka raia wa Goma.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangaza kuwa atakatisha safari yake barani Ulaya na kurejea nyumbani leo kushughulia janga hilo.

Kwa ujumla hali ya taharuki imetanda kote Goma huku wengi wasijue wakimbilie wapi.

342/